WATANZANIA MILIONI 37 KUPIGA KURA TAREHE 29 OKTOBA, 2025

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.

Sehemu ya viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyohudhuria hafla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.

Sehemu ya viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyohudhuria hafla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.



******************
Na. Mwandishi Wetu
Tarehe 29 Oktoba, 2025 ndio siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara. Jumla ya Wapiga Kura 37,655,559 wamejiandikisha.
 
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele leo tarehe 26 Julai, 2025 kwenye hafla ya uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi iliyofanyika kwenye makao makuu ya Tume, Njedengwa jijini Dodoma.
 
“Tarehe 09 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais. Tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani na tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani,” amesema Jaji Mwambegele na kuongeza…..
 
“Tarehe 28 Agosti, 2025 hadi tarehe 28 Oktoba, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara. Tarehe 28 Agosti, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema na Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndiyo Siku ya Kupiga Kura”.
 
Akazingumza kuhusu idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huo, Jaji Mwambegele amesema jumla ya wapiga kura 37,655,559 wamejiandikisha na kuongeza kuwa idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwa kwenye daftari, mwaka 2020.
 
Ameongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, Wapiga Kura 725,876 wapo katika Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.
 
“Katika idadi ya wapiga kura 37,655,559 waliopo katika daftari, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapiga kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Ameongeza kuwa kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69 na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu.
 
Amesema jumla ya vituo 99,911 vitatumika kupigia kura ambapo vituo 97,349 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Bara na vituo 2,562 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar.
 
“Idadi hii ya vituo 99,911 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020,” amesema.
 
Jaji Mwambegele ametoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume.

No comments