Serikali Yasisitiza Haki, Uwazi na Uadilifu kwa Wafanyabiashara

Wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo wametakiwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uadilifu katika utekelezaji wa shughuli zao ili kuhakikisha biashara zinafanyika katika mazingira yenye tija na ushindani wa haki. Wito huo umetolewa leo Machi 3, 2026, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara kuhusu haki na wajibu wao katika kukuza uchumi wa nchi.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeo Manongi, amesema wafanyabiashara wana jukumu kubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla. Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni msingi muhimu wa mafanikio ya kiuchumi.

Manongi ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha sera, sheria na kanuni ili kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. Amesema mifumo ya ushindani wa kibiashara imeimarishwa ili kuhakikisha hakuna upendeleo unaoweza kudhoofisha soko huria.

“Serikali imeweka mazingira mazuri ya ushindani wa kibiashara na inatambua kuwa uchumi wa nchi unategemea usawa kwa wadau wote,” amesema Manongi. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara kuzingatia maadili na taratibu zilizowekwa ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Aidha, amewahimiza wafanyabiashara kutumia fursa za mafunzo na semina zinazotolewa mara kwa mara na Serikali ili kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya kisheria, ushindani na haki za kibiashara. Amesema elimu hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi yatakayokuza biashara zao kwa muda mrefu.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira ya biashara yanabaki kuwa rafiki na yenye ushindani sawa kwa wote, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa Tanzania na kuongeza ajira kwa wananchi.




 

No comments