SERIKALI YAIELEKEZA TPSC KUONGEZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUIMARISHA UTUMISHI WA UMMA
Dar es Salaam, Julai 3, 2026,
Serikali imekielekeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuendelea kuongoza matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence), katika kuandaa watumishi wa umma wenye uwezo wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya TPSC yaliyofanyika katika Julius Nyerere International Convention Centre, jijini Dar es Salaam
Kikwete amesema mabadiliko ya haraka ya teknolojia duniani yanahitaji taasisi za umma kwenda sambamba na maendeleo hayo ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Serikali inatarajia kuona Chuo hiki kikiongoza juhudi za kuandaa watumishi wa umma watakaoweza kutumia teknolojia za kidijitali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wa Serikali," amesema Kikwete.
Aidha, Kikwete mesema, katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, chuo kimepiga hatua kubwa za maendeleo kwa kuongeza kampasi kutoka mbili hadi sita, kupanua programu za mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, kuanzisha mafunzo kwa njia ya mtandao, pamoja na kuimarisha tafiti tumizi na huduma za ushauri wa kitaalamu.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haraka na zenye tija.
Akitoa taarifa ya miaka ishirini na tano ya Chuo, Chuo, Mkuu na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema Chuo kilianzishwa mwaka 2000 kwa lengo la kuleta mageuzi katika utumishi wa umma nchini kupitia mafunzo, tafiti na huduma za ushauri wa kitaalamu.
Dkt. Mabonesho amesema katika kipindi cha miaka 25, Chuo kimefanikiwa kupanua huduma zake kwa kuongeza idadi ya kampasi kutoka mbili hadi sita, kuboresha programu za mafunzo na kuanzisha mfumo kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha watumishi wa umma kupata mafunzo popote walipo.
"Upanuzi huu umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha mafunzo na huduma za kitaalamu," amesema Dkt. Mabonesho.
Aidha ameongeza kuwa, kuwa TPSC itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa, tafiti tumizi na ubunifu ili kuendelea kuzalisha watumishi wa umma wenye ujuzi na uwezo wa kukidhi mahitaji ya Serikali na maendeleo ya Taifa.




















Post a Comment